Saturday, July 26, 2014

FIGO: MATATIZO YAKE, TISHIO KWA MAISHA YA WATANZANIA

Front view of Urinary Tract

Kidney


Hapa duniani kuna maradhi aina nyingi yanayotisha, yakisumbua binadamu, kuwatia ulemavu hata kuwa chanzo cha uchumi kutetereka, wakati mwingine kusababisha kifo. Miongoni mwa maradhi hayo ni kuharibika kwa figo.
Ugonjwa huo unaelezewa kwamba siyo tu unaleta maumivu kwa mgonjwa, bali pia hautibiki kirahisi pamoja na gharama za matibabu husika kuwa kubwa na wengi kushindwa kuzimudu.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa, zipo sababu kadhaa zinazosababisha maradhi katika figo kwa binadamu ikiwamo matumizi mabaya ya dawa hasa za maumivu, dawa za kienyeji, baadhi ya dawa za Kichina, uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Onesmo Kisanga, Daktari Bingwa wa Figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH), Kitengo kinachoshughulika na tiba ya usafishaji wa figo na damu(Renal Dialysis Unity) anasema kuwa tiba ya usafishaji wa figo kwa kitaalamu (Dialysis), uhusika na utoaji wa maji yaliyojaa mwilini, uchafu, pia sumu zitokanazo na vyakula au dawa. Dk Kisanga anasema kuwa tiba ya 'Dialysis' ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji kuipata, hutakiwa kutoa kiasi Sh300, 000, huku akitakiwa kuipata tiba hiyo angalau mara tatu kwa wiki ambapo hugharimu Sh900,000.
"Hii huduma inafanyika hapa (MNH) katika Kitengo cha Renal Dialysis Unity, na mgonjwa anatakiwa kuipata tiba hiyo maisha yake yote,"anasema Dk Kisanga.
Anafafanua kuwa Dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitaji kutoka kwenye damu ya mtu. Mchakato huo hufanyika baada ya figo kushindwa kufanya kazi na taka hizo kuingia kwenye mfumo wa damu. Kwa kawaida figo hufanya kazi ya kuchuja uchafu katika mwili, lakini baadhi ya watu huathirika na figo zao kushindwa kufanya kazi ya kuchuja uchafu huo kutokana na sababu mbalimbali zilizoainisha awali.
Kwa mujibu wa Dk Kisanga, usafishaji wa figo hufanywa kwa wagonjwa ambao figo zao zimeathirika kwa kiasi kikubwa na maradhi au hata kwa dharura.
Anafafanua kuwa mgonjwa hutundikiwa mipira maalumu, huku kwenye mashine kukiwa na figo ya bandia ambayo kazi yake ni kupitisha damu, kuisafisha na kuirudishwa mwilini.
Anaelezea kuwa kwenye mashine maalumu kunakuwa na mipira kadhaa ikiwamo ya kupitishia damu kupeleka kwenye figo bandia, inayofanya kazi kama ya mwilini na mirija mingine ambayo ni mikubwa kiasi inatumika kutoa maji yasiyohitajika mwilini na sumu, huku mingine ikitumika kurudisha damu safi mwilini.
"Mgonjwa hulala akifanyiwa tiba hii kwa saa nne, bila kuchomwa sindano ya usingizi, kwa kuwa haina maumivu makali. Vilevile mgonjwa hutobolewa eneo maalumu mwilini kwa ajili ya kupitishia mipira. Kuna wanaotobolewa shingoni au mkononi kulingana na anavyotaka mgonjwa," anasema Dk Kisanga.
Anaongeza kuwa pamoja na tiba hiyo kuwa ghali, bado haina uhakika wa kupunguza tatizo kwa asilimia 100, bali kwa asilimia 40 hadi 50 pekee.
Mtaalamu huyo wa afya anaitaja tiba nyingine kuwa ni ya kupandikiza figo, (kidney transplant) ambayo kwa sasa haifanyiki nchini. Hata hivyo ili kufanyiwa upandikizaji huo nje ya nchi, mgonjwa anahitaji zaidi ya Sh20 milioni.
"Tiba hii hufanywa hasa kwa mgonjwa ambaye figo yake imekufa na haiwezi kufanywa tena nchini," anasema Dk Kisanga.
Madhara ya tiba hizo
Hata hivyo, Dk Kisanga anasema kuwa tiba ya figo ina madhara kiafya hasa kwa walio kwenye hatua ya tano ya tiba hiyo. Madhara hayo ni pamoja na maradhi ya moyo, miguu kukaza na maumivu ya kifua.
Kazi kuu za figo mwilini
Dk Kisanga anaeleza kuwa figo ni miongoni mwa viungo muhimu katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu.
Anasema kuwa kwa kawaida, mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu.
Anazitaja kazi kuu za figo kuwa ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu katika damu, kusaidia kuhifadhi,kudhibiti kiwango cha maji na madini (electrolytes) mwilini.
Figo huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika.
Anaendelea kuwa kazi nyingine za figo ni pamoja na kusaidia kutengeneza kiasili cha erythropoletin ambacho ni muhimu katika utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu, hupokea asilimia 25 ya damu na kila figo ina chembechembe hai ndogo milioni moja, pia kusaidia kudhibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure).
Aina za ugonjwa wa figo
Dk Kisanga, anazitaja aina za ugonjwa huu kuwa ni mbili; ya kwanza ni ile ya figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla na muda mfupi; pili ni ile ya figo kushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu.
Figo kushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu.
Daktari huyo anasema kwa aina hii ya ugonjwa, figo huharibiwa taratibu na kuendelea kupunguza uwezo wake wa kufanya kazi kadiri siku zinavyokwenda.
Dalili za aina hii ya ugonjwa huchelewa kujitokeza na wakati mwingine mwenye tatizo hajisikii dalili yeyote, hadi pale inapotokea akaugua ugonjwa mwingine na daktari kuhisi tatizo, ndipo hugundulika kuwa na ugonjwa huo baada ya vipimo.
Sababu za figo kushindwa kufanya kazi ghafla
Dk Kisanga anaitaja sababu kubwa ni kupungua kwa mzunguko wa damu kwenye figo, kemikali za mwilini au kushambuliwa na sumu.
"Kushuka kiwango cha mzunguko wa damu humpata mtu ambaye anatapika sana na hanywi maji ya kutosha, anayeharisha sana na hanywi maji ya kutosha na wale ambao hupoteza damu nyingi kama vile kwenye ajali," anasema Dk Kisanga.
Dk Kisanga anazitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo, moyo kushindwa kusukuma damu kwa ghafla, au waliougua maradhi ya moyo kwa muda mrefu.
Kisanga anazitaja kemikali kuwa ni pamoja na zinazotokana na kutumia dawa iliyo na mzio kwa mtumiaji, dawa zinazosababisha mkojo utoke kwa wingi, dawa za kienyeji na baadhi ya dawa za malaria.
"Tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla pia humpata mtu ambaye ana bakteria kwenye mzunguko wa damu, ambao wanaweza kusababisha homa 'Septicemia' na kuugua malaria," anasema Dk Kisanga.
Anazitaja sababu zinazofanya figo ishindwe kufanya kazi taratibu na kwa muda mrefu na hatimaye kushindwa kabisa kuwa ni presha kuwa juu, kisukari, magonjwa yanayosababishwa na bakteria, HIV, saratani na sumu mbalimbali zinazoingia mwilini.
Dalili za figo kushindwa kufanya kazi vizuri
Dk Kisanga anasema kuwa dalili ya kwanza ni kupungua kwa kiasi cha mkojo, kushindwa kupumua, kusikia kichefuchefu, kutapika na kuvimba miguu.
Nyingine ni maji kujaa mwilini, madini ya mwili kuwa juu hasa ya 'potashiamu', asidi nyingi, matatizo katika moyo, ubongo, kukosa hamu ya kula na kudhoofika mwili.
Anazitaja dalili nyingine kwa wagonjwa ambao hawagunduliki mapema ni kuvimba macho wakati wa asubuhi na uvimbe kupungua baadaye.
Nyingine ni kuvimba miguu asubuhi, kupungukiwa damu mwilini kama dalili za kwanza (kwani figo ikishindwa kufanya kazi ya kusaidia kutengeneza damu).
Ushauri
Dk Kisanga anasema kuwa wakati tukielekea Siku ya Figo Duniani ambayo hufanyika tarehe 13 Machi ya kila mwaka, ni vyema jamii ikaelewa kuwa figo ni ogani inayohitahi utunzaji wa hali ya juu.

0 comments:

Post a Comment