Friday, April 12, 2013

JINSI YA KUPANGILIA NA KUTUMIA MUDA WAKO VIZURI!

MAMBO SABA (7) MUHIMU YA KUZINGATIA:

 

Bila shaka umeshawahi kusikia msemo wa wenzetu wa magharibi usemao “Time is Money”. Yawezekana kwamba msemo huo,kwa tafsiri ya moja kwa moja, unamaanisha kwamba muda ni pesa. Lakini ninavyoelewa mimi msemo huo unaongelea au unajaribu tu kuonyesha jinsi gani muda ni kitu cha thamani! Jinsi unavyoutumia muda wako hivi leo ni ishara tosha ya jinsi kesho yako itakavyokuwa.
Kwa upande mwingine umeshawahi kusikia mtu au watu fulani fulani wakilalamika kwamba “hawana muda” wa kufanya kitu fulani. Sababu itolewayo mara nyingi ni kwamba wapo “bize”. Wapo ‘bize” na ndio maana hawana muda wa kujitolea katika shughuli mbalimbali za kijamii.Ndio maana hawana muda wa kikao cha harusi cha rafiki,ndugu au jamaa.Hawana muda wa kuhudhuria msiba wa mtu. Wapo “bize” na ndio maana hawakuweza kukupigia simu nk.
Sasa inakuwaje mtu mmoja awe na muda na wakati huo huo mtu mwingine asiwe kabisa na muda wakati sote tunaishi kwenye dunia moja na siku ina masaa yale yale 24? Sababu zinaweza kuwa nyingi. Zingine zinaweza kuwa ni za visingizio tu.Zingine zinaweza kuwa za kweli na za uhakika.
Pamoja na hayo, jinsi unavyotumia muda wako, jinsi unavyopangilia mambo yako, ratiba zako nk, ni sababu ya kutosha kama una muda wa ziada wa kufanya mambo mengine mengi uyapendayo ikiwemo mapumziko, muda wa kukaa na wanafamilia yako, kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni na lolote lile ambalo unapenda kulifanya lakini umekuwa hulifanyi kwa sababu au kisingizio cha ukosefu wa muda.
Leo tutaangalia baadhi ya mambo ambayo unaweza kuyafanya ili kuokoa muda ili kujipatia muda unaohitaji kwa sababu ambazo nimezitaja hapo juu;

    

  • Anza siku yako mapema: Hili ni la msingi sana.Amka mapema. Ukiianza siku yako mapema, sio tu kwamba kuna faida za kiafya kama ambavyo tutakuja kuziongelea katika siku za mbeleni, bali unakuwa na muda wa ziada wa kuiandaa ratiba kamili ya siku yako. Kwa ujumla binadamu anatakiwa kulala kwa muda wa masaa nane. Siri ya kuamka mapema inaanza na kwenda kulala katika muda unaofaa ili upate hayo masaa manane. Kumbuka siku njema huonekana asubuhi.Ipe siku yako mwanzo mzuri.
  • Orodhesha mambo unayotaka kufanya: Ushasikia msemo usemao; Mali bila daftari hupotea bila kujua. Hali ni hiyo hiyo hata katika suala zima la muda. Unapoianza siku hakikisha umeorodhesha mahali kwenye kikaratasi au kidaftari chako cha kumbukumbu mambo yote ambayo umedhamiria kuyafanya katika siku inayokukabili.Katika zama hizi za sayansi na tekinolojia,simu nyingi za viganjani zina huduma ya kalenda ambayo unaweza kuitumia kuorodhesha mambo unayotaka kufanya kesho,mwezi ujao au hata mwakani.Zitumie.Andika pia na muda ambao ni lazima utimize mambo hayo.
Faida za kuorodhesha mambo unayotaka kufanya ni kwamba kwanza orodha hiyo itakuwa inakusuta. Itakuwa inakuuliza,ulisema leo utafanya hivi imekuwaje? Pili orodha hiyo hiyo itakupa pia nguvu au ari ya kutimiza malengo yako. Tatu na muhimu zaidi kama mada yetu ya leo inavyodai, utaokoa muda. Utafanya kila jambo kutokana na muda uliojipangia kwani orodha itakuwa inakuonyesha kwamba siku bado haijaisha na mengine yanakungoja.
Pia wakati unaandika orodha yako, kumbuka kuweka pamoja mambo ambayo yanaweza kufanyika kwa pamoja au katika muda huo huo.Kwa mfano, leo umepanga kwenda katika benki fulani kuomba mkopo wa biashara.Wakati huo huo umepanga kwenda kwa chakula cha mchana na rafiki yako anayefanya kazi katika benki hiyo hiyo. Hayo unaweza kuyatimiza kwa pamoja. Unaweza kumuona meneja wa mikopo wa benki na kisha baada ya kumaliza ukaenda na rafiki yako kupata chakula. Hakikisha tu kwamba rafiki yako sio huyo huyo tena ndio meneja wa mikopo.Hapo kutakuwa na harufu ya ufisadi.Unajua tena jinsi mambo yalivyo nchini mwetu hivi sasa.Kuwa makini.
  • Weka kipaumbele: Hili linaendana moja kwa moja na hilo hapo juu. Unapoandika orodha yako, weka kipaumbele katika mambo ambayo ni muhimu zaidi.Hayo yaweke juu kabisa katika orodha yako. Kipaumbele kinaweza kutokana na umuhimu wako binafsi kwa jambo fulani, muda nk
  • Jifunze kutoahirisha mambo: Mara nyingi huwa tunakamatwa na uvivu na kusema hili nitalifanya kesho au keshokutwa.Tunasema linaweza kusubiri. Ukweli ni kwamba ni kweli jambo hilo litasubiri. Cha msingi kukumbuka ni kwamba jambo hilo litaendelea kukusubiri mpaka hapo utakapoamua kulifanya! Haliendi popote.Ushauri wangu ni kwamba ule ambao hata wazee wetu walipenda kutukumbusha,Linalowezekana Leo Lisingoje Kesho.Unapoahirisha kutimiza jambo fulani kumbuka kwamba unazidi tu kuongeza mambo katika orodha yako ya kesho au keshokutwa. Huo ndio mwanzo wa kuchanganyikiwa, kukosa kabisa muda wa kufanya yale uyapendayo zaidi maishani zaidi ya kazi na kutafuta hela.
  • Muda na marafiki:
    Kama nilivyosema hapo mwanzoni, mada ya leo ni kujaribu kuona jinsi gani mtu anaweza akaokoa muda ili apate muda wa kuwa karibu zaidi na ndugu,jamaa na marafiki katika mambo ya kijamii nk. Lakini utashangaa nikikuambia kwamba marafiki pia wanaweza kuwa chanzo kizuri cha matumizi mabaya ya muda wako?Liangalie hili kwa makini kwani inategemea sana na aina ya marafiki na jinsi mnavyoamua kutumia muda wenu.
Kwa mfano kama una rafiki ambaye hazingatii muda,hana miadi ya uhakika huyo anaweza kuwa mzigo katika suala zima la matumizi ya muda. Angalia kwa makini urafiki wenu. Jaribu kumuelekeza mwenzako kuhusu umuhimu wa muda katika ratiba na mipangilio yenu.Naamini ataelewa. Pia jaribu kuangalia,mnapokutana kama marafiki,mnatumiaje muda wenu? Je mnatumia muda huo kupanga mikakati ya maana ya maisha au mnaishia tu kusengenya watu na kupiga umbea? Sihitaji kukuambia kitu zaidi.Unajua cha kufanya.
  • Fanya jambo zaidi ya moja kwa wakati mmoja: Kwa kiingereza hili linaitwa “Multi-tasking”. Yapo mambo ambayo unaweza kuyafanya kwa wakati mmoja. Mifano ipo mingi. Kata kucha zako ukiwa unaangalia televisheni, sikiliza taarifa ya habari huku ukiandaa nguo zako za kuvaa kesho kazini. Unaweza pia kujibu barua pepe zako wakati unapata kifungua kinywa.Mifano ipo mingi. Cha msingi ni kuhakikisha kwamba hayo mambo mawili unayojaribu kuyafanya yanawezekana kufanyika kwa wakati mmoja na pia ni salama kufanya hivyo.Kwa mfano sikushauri uongee kwenye simu ya mkononi wakati unaendesha gari.Sikushauri utumie chombo chochote cha umeme wakati ukifanya shughuli zingine.Angalia usije kuwa kama yule jamaa ambaye alikuwa anapiga pasi,simu ikaita.Badala ya kupokea simu,akapokea pasi! Ni hatari.
  • Jipange, pangilia ratiba: Ukipenda unaweza kusema hili la kujipanga na kupangilia ratiba ni mkusanyiko wa yote niliyotaja hapo juu. Muda mwingi sana huwa tunaupoteza kutokana na kutopangilia vizuri mambo yetu,ratiba zetu za kila siku. Upo umuhimu kwa mfano wa kupangilia shughuli zetu kutokana na sehemu za kijiografia.Kwa mfano kama una shughuli ambazo zinahitajika kufanyika mjini(siku hizi huwa Napata tabu kubainisha wapi ni mjini), hakikisha kwamba unapokwenda mjini unazikamilisha zote kwa wakati mmoja. Haingii akili kwanini mtu aende mjini zaidi ya mara tatu kwa siku.Kwanini alipoenda mjini asubuhi asingefanya yote aliyotakiwa kuyafanya? Hali ni hiyo hiyo hata majumbani mwetu. Utakuta mtu amefanya safari zaidi ya mia mbili kutoka chumbani kwenda jikoni. Kwanini? Jibu rahisi ni ukosefu wa mpangilio.
Mbinu za kuokoa muda ni nyingi zaidi ya hizi chache ambazo nimeziorodhesha. Unaweza kuongezea katika orodha hii.Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba yawezekana kabisa kupata muda wa ziada wa kufanya mambo uyapendayo maishani. La msingi ni kuwa na mpangilio wa muda.Tumia mbinu hizi na zinginezo ili kufanikiwa katika suala la muda.Usilale zaidi ya masaa manane kwa siku. Muda ni zawadi kutoka kwa muumba.Utumie vizuri.

0 comments:

Post a Comment