SURA YA KWANZA:
Anza kujipanga:
Ili upate mafanikio siku zote unahitaji shauku ya dhati
katika kufanikisha hilo
sanjali na mkakati wa vitendo. Kuwa na shauku ya dhati itakusaidia kufanya
mambo yako kwa vitendo zaidi, sababu vitendo ndiyo mafanikio yenyewe,
ukizingatia hili mafanikio yatakuja kama
ambavyo wewe unataka. Lakini je, ni kweli una hamu ya mafanikio katika maisha
yako? Ndo swali la kujiuliza, kama jibu ndiyo,
je, mipango yako ipo wapi? Unataka
kufanikiwa nini katika maisha? Na kwa vipi utafanikiwa? Unafanya nini ili
kupata hayo mafanikio? Je, upo tayari
kubadili mfumo wa maisha yako? Upo tayari kuyafuatilia malengo yako? Na je, upo
tayari kutathimini malengo yako mara kwa mara? Hayo ni maswali mengine
unayopaswa kujiuliza pia.
Kuishi maisha ya mafanikio ina maana ni hali unayokuwa
umeitafuta, inaweza kukuchukua miaka kuifikia au kukamilisha malengo yako kama tu utaendelea kuweka hai ndoto zako za mafanikio.
Fomula ya mafanikio ni rahisi lakini unashindwa kufanikiwa sababu hauna shauku
ya dhati ya kutaka kufanikiwa au hauna mkakati madhubuti kufikia malengo hayo. Kwani
kama unataka kufaulu mtihani ni lazima usome kwa bidii, na kama
unataka kuwa na afya njema ni lazima ufanye mazoezisana.
Hilo
ndilo unalotakiwa kufanya hata unaposaka mafanikio, lazima ufanye jitihada ili kufikia
mafanikio hayo. Na pia ili ufanikiwe unahitaji kujifunza mbinu mpya za
mafanikio, hakuna jinsi kwa sababu hakuna njia ya mkato katika hili.
Kama unaifanyia kazi shauku yako ya kutaka kufanikiwa na
unakuwa na mkakati madhubuti, ni wazi mafanikio utayaona na yatakuja kama ulivyopanga.
Ni muhimu kujifunza kupitia uzoefu wako katika maisha kwani
maisha ndiyo mwalimu mkubwa wa kukuongoza. Kila hatua unayopitia katika kusaka
mafanikio inakupa wazo jipya, na kama hupati
wazo jipya basi tambua kwamba unapitia hatua zisizofaa.
Siku zote mafanikio yanachochewa na mawazo mapya unayoyapata
katika kila hatua unayopitia unaposaka mafanikio.
Watu wengi hujifunza kupitia maisha, kwani busara ndiyo
hutumika kupambana na vikwazo vinavyojitokeza katika harakati za kusaka
mafanikio.
Pia ni muhimu sana
kuyafanyia kazi mawazo mapya unayoyapata katika kila hatua unayopiga kwenye
kusaka mafanikio.
Endelea kuyafanyia kazi mawazo hayo kila mara kwa kuwa bila
kufanya hivyo unaweza kupoteza malengo yako.
Mafanikio siyo ushirikina lakini unaweza kujikuta unaingia
huko kusaka mafanikio, kama hauna mikakati ya
kweli kwa ajili ya mafanikio.
Jipange kufikia mafanikio ambayo tayari unayo ila tu hujui
namna ya kuyapata.
Kila mtu amefanikiwa ila namna ya kuyaona mafanikio hayo
ndiyo inayomsumbua kila mmoja wetu. Na kama utatulia ukajipanga vyema huku
ukipangilia malengo yako ni wazi mafanikio utayaona bila tatizo lolote, kwani
waliofanikiwa walikuwa kama wewe tu. Kwahiyo
anza sasa kuyasaka mafanikio kwa nguvu zote hujachelewa bado.
Njia kubwa ya kupata mafanikio katika maisha ni kujua namna
ya kutumia vyema mawazo, akili yako na upeo wako wa kufikiri katika kusaka
mafanikio.
Upeo wako wa kufikiri ndiyo unaozalisha mawazo ambayo
hukusaidia katika kufanikisha mambo mbalimbali unayoyahitaji katika maisha.
Ingawa kuna wakati unaacha kufanyia kazi mambo mema na
kuruhusu yasiyo mema kutawala mawazo yako na kugeuza mambo ya kweli katika
maisha yako ya kila siku.
Akili yako ni kama kiwanda
cha kuzalisha yale yote unayoyataka.
Ni jukumu lako kuhakikisha unatawala na kutumia ipasavyo
akili, mawazo na upeo wako wa kufikiri kwa ujumla katika kusaka mafanikio.
Kama kweli utaweza kutumia
akili yako, ni wazi utashangaa namna
ambavyo mafanikio yatakavyokuwa yanakuja kwa urahisi kwako bila hata kutumia
njia zisizo sahihi.
Kuwa na matarajio ya dhati katika yale mambo ya msingi,
kwani hayo ndiyo mambo unayotakiwa kuyafikiria katika akili yako huku ukijenga
picha halisi ya jambo unalolifikiria.
Kwa kufanya hivyo utaona fursa nyingi zinajitokeza mbele
yako na kwa kuwa utakuwa na matarajio nazo hautakuwa na muda wa kupoteza katika
kuzitumia fursa hizo.
Watu wengi huwa na mawazo ya kufanikisha ndoto zao na
kutamani ndoto hizo kuwa kweli kwa muda mfupi, jambo hili linawezekana ingawa
si kwa muda mfupi kama wengi wanavyotaka.
Chukua muda kufanyia kazi mawazo yako, vinginevyo utakuwa mtu wa kufikiria vitu
tu bila kuvifanyia kazi.
Kitu ambacho unaweza kukiongoza katika maisha yako ni kile
unachokiingiza katika akili yako pamoja na mawazo uliyonayo akilini mwako.
Akili yako inafanya kazi jinsi unavyoiongoza, kama utaiongoza katika uoga hivyo ndivyo itakavyofanya
kazi pia.
Lakini kama una mawazo mema na yenye mtazamo wa mafanikio
basi hauko mbali na malengo na ndoto zako, hii ni kwasababu tu unaongoza vyema
mawazo yako.
Na kama unajua unachokitaka
lakini ukaruhusu mawazo mabaya yatawale akili yako basi tambua kwamba
hautafanikiwa.
Kujua unachokitaka na
kujua kufikiria, ina maana mafaniko kwako yatakuja kama
ulivyopanga na mwanga utauona katika maisha yako.
Jitahidi kuyaepuka mawazo mabaya, kaa mbali na watu ambao
wanaweza kuchangia mawazo mabaya ambayo
yatakuondolea mawazo ya kimafanikio.
Fikiria mawazo mapya, jua unachokitaka , tazama mafanikio
yako yanafananaje, tafuta mawazo yatakayokufanya uwe katika muongozo wa
mafanikio.
Suala hili linahitaji moyo na mtazamo wa kweli kufanya
mawazo mazuri kuwa tabia yako na mfumo wa maisha yako.
Siri ya kufanikiwa katika maisha yako ni kufikiria mafanikio
tu, mbali na hilo
mawazo mazuri yatakufanya uwe na uchaguzi mzuri katika mambo yako
utakayoyafanya kwa ajili ya mafanikio.
Mafanikio hutokea pindi unapokuwa umejikita katika malengo
na ndoto zako na kuhakikisha ndoto na malengo vinatimia.
Mtu anayesaka mafnikio hachoki kufanya kazi kwa sababu haoni
kama anafanya kazi, hii sababu anaipenda kazi yake au anapenda anachofanya au anafanya
anachopenda.
Siri nyingine ya kupata mafanikio ni kuwa muwazi kila mara
ili uweze kupambana na changamoto mpya, kwa sababu hauko sahihi wakati wote,
inamaana utakuwa unajifunza kila mara. Mafanikio unayo ndani ya mawazo yako,
kumbuka kama utashindwa kutumia uwezo wa akili
na mawazo mazuri uliyobarikiwa na muumba basi ni wazi mafanikio kwako
hayatapatikana katika hali uliyoitarajia.
Mafanikio hayaji bila kufanya kazi kwa bidii, na ili
ufanikiwe unahitaji kuwa na malengo, si rahisi kuwa na mafanikio katika maisha
kama huna malengo, kwani ni rahisi sana kuwa na mafanikio kama una
malengo.
Ili uweze kufanikiwa katika
maisha ni lazima uamini kuwa unaweza kufanikiwa, bila ya kuwa na imani hiyo
huwezi kufanikiwa kwa kuwa tayari hutakuwa na ari ya kufanikiwa.
Mafanikio hayaji kwa siku moja ni lazima uyatafute kwa
kufanya kazi kwa bidii na nidhamu, bila vitu hivyo ni vigumu kufanikiwa.
Unaweza kufanya kazi kwa bidii kila siku katika maisha yako
lakini bila ya kuwa na nidhamu na kile unachokipata katika kazi zako huwezi
kufanikiwa, ili uweze kufikia malengo yako ni muhimu kudhibiti na kutumia kwa
uangalifu chochote unachokipata katika shughuli zako.
Pia ni lazima uwe mtu ambaye unatambua kuwa wewe ni nani
katika dunia hii na maisha yako kwa ujumla. Kwa kufanya hivyo utakuwa unajua
unahitaji nini katika maisha yako, lazima pia uzingatie ulikotoka kwani maisha
yako ya awali yana mafundisho mengi sana
ambayo ukiyatumia kujfunza itakusaidia kupata mafanikio yako binafsi.
Baadhi ya watu huogopa kukumbana na changamoto lakini ni
muhimu kufahamu kuwa katika maisha kushindwa au kukutana na changamoto zozote
zile ni kama kuiona fursa nyingine mbele yako.
Kama utakuwa unatumia changamoto hizo
kujifunza vitu vipya kila siku basi itakusaidia kwa kiasi kikubwa katika harakati
zako za kutafuta mafanikio.
Wengi wanaogopa kushindwa au kukutana na mitihani kwa sababu
wanahisi itawaumiza mioyo yao,
na pengine hata kuivunja kabisa.
Lazima tufahamu kuwa hata dunia huwa na majira yake ambayo
huleta mabadiliko katika maisha yetu, na mabadiliko hayo huwa tunakabiliana
nayo katika hali yoyote ile ambayo majira hayo yatakuja nayo.
Vivyo hivyo na hali ya kushindwa au kukutana na changamoto, vitu
hivyo viko katika maisha yetu ya kila siku na yanaweza kuja katika hali tofauti
kulingana na wakati.
Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anachukulia kushindwa
kwake au kuzitumia changamoto anazokutana nazo katika njia zake za kuelekea
kwenye mafanikio kuwa ni fursa mpya zinazojitokeza na hana budi kuzikubali na
kuzitumia kupata mafanikio.
Wengi hatujui ni nini
kilichomo katika maisha yetu, na ili kujua tulichojaaliwa ndipo hapo suala la
kushindwa au kukutana na changamoto huwa tunaliweka kando.
Maumivu ya kushindwa tunayoyapata huchangia katika
kutuhamasisha tusikate tamaa ila tuendelee kutafuta kile tulichojaaliwa ndani
yetu na kuweza kukitumia kupata mafanikio.
Bila kushindwa au kukutana na changamoto, hatuwezi kuwa na
moyo wa kufanya jambo lolote la kimaendeleo na kutimiza ndoto zetu za kupata
mafanikio.
Chukulia changamoto kuwa ni mwanzo wa kitu kipya na ambacho
ni bora zaidi, na usichukulie changamoto kama
ndio mwisho wa safari yako ya mafanikio.
Unaweza kupata chochote katika maisha kama
tu una nia ya kutumia fursa zilizopo kupata hicho unachokihitaji.
Ndoto yoyote inayotawala mawazo yako huishia kuwa kweli, na
mwishowe utapata matokeo mazuri. Hebu fikiria juu ya watu waliopata mafanikio,
unafikiri walilala wakaamka na kuwa na mafanikio waliyonayo leo, hapana
walihangaika na kukutana na vikwazo tele.
Kwanza walikuwa na mitazamo chanya juu ya kile walichokuwa
wakikiota na kukiwaza siku zote, ni nadra sana
kumkuta mtu aleyefanikiwa akisema siwezi au jambo hilo
gumu sana
kulifanya. Lakini angalia watu wasio na
mafanikio mara kwa mara huongea katika hali ya kukata tamaa na maneno yao huwa siwezi au jambo hilo ni gumu kulifanya.
Lakini ni uchaguzi wako, chochote unachokifanya kinaamuliwa
na mawazo yako, la
msingi ni kujipanga na siyo kulaumu watu, hii ni kwa ajili
ya mustakabali wako.
Siri ya kuwa mwenye nguvu katika jamii ni moja tu, nayo ni
kufanya vitu kwa nguvu, usahii na umakini mkubwa ili wengine wakuamini bila
kukutilia mashaka yoyote.
Tatizo kubwa ni kwamba miongoni mwa wengi ni kutaka kuwa na
nguvu bila kutenda mambo kwa usahii. Tufahamu kuwa ukitaka kuwa na ushawishi
lazima watu wakuamini, ili wakupende unatakiwa kuishi kwa wema, ili uwe na
marafiki inabidi uwavutie kwa tabia zako uwe mwana jamii wa kujitolea, ujuzi
utafute kwa kusoma na kujifunza kila siku, mafanikio yatafute kwa kujishughulisha
kwa bidii sana bila kuchoka.
Jamii ikikuamini kwa matendo yako utakuwa na nguvu tu.
Siku zote kumbuka kwamba ili upate unachokihitaji inabidi
kwanza uamue kukipata.
Na tena ni lazima ujue ni nini haswa unataka, ndipo na akili
yako itajua unataka nini.
Pia ni vizuri kuandika kwenye karatasi ili iwe rahisi kwako
kukumbuka, kwani kila kitu kipo akilini na hapo ndipo kila kitu huanzia. Unapojua
kile unachokihitaji hiyo ndio hatua ya kwanza katika kukipata.
Tambua ya kwamba unaposhindwa kupanga basi unapanga
kushindwa kila kitu.
Usiogope kujaribu kwani binadamu kazaliwa ili afanye makosa,
kwa kuwa nguvu mbili za mema na maovu ndani ya mwili wake zinashindana, hivyo
ataendelea kusumbuka mpaka pale nguvu moja itakapomshinda mwenzake ndipo
ushindi upatikana.
Jinsi wenzetu wanavyotuathiri
katika maisha yetu
Hakuna binadamu aliyezaliwa Malaya,
jambazi, mwizi nk. Wote kwa namna zetu tumekuwa tulivyo kwa sababu ya harakati
za maisha.
Pengine litakuwa swali la msingi kujiuliza kwanini kusiwepo
na aina moja tu ya binadamu, tofauti na tuonavyo leo ikiwa wote tumezaliwa
wasafi?
Je, kati yetu wapo waliopenda kuwa vile walivyo [yaani
wahalifu, Malaya,
wavuta madawa nk.] ? Tafiti hazioneshi kwamba wahalifu walichagua tabia hiyo,
wengi kati yao hawakumbuki ni lini ilikuwa siku yao ya kwanza
kujitumbukiza kwenye tabia hizo chafu.
Kama hilo halitoshi miongoni
mwa watu waliofungwa na tamaa za ngono
walifanyiwa utafiti walionesha kutojua mwanzo wa tabia zao na kufanya kuwe na
jambo la kujiuliza tena, kwanini hawajui na iweje wasikumbuke vitu
walivyochagua kuvifanya katika maisha yao?
Katika hali ya kawaida umalaya ni nembo{utambulisho wa mtu/
kitu} kama watengeneza bidhaa wanavyofanya wanapozalisha mali zao.
Ili mtu ajue kwamba ile ni
bidhaa Fulani lazima mtengenezaji achukue jukumu la kuiweka jina na kuibandika
ili kumuwezesha mtu kuitambua.
Hata mungu katika uumbaji wake alivitambulisha vitu kwa
nembo kama tunavyoviita leo. Hebu tujiulize
tena ni nani aliyewawekea nembo majambazi, makahaba nk. tunaowaona leo mpaka
jamii ikafikia hatua ya majina hayo? Hapa kuna haja ya kujifunza zaidi.
Siku zote waweka nembo ni watengenezaji bidhaa, hivyo
wakiwepo majambazi, wezi na makahaba miongoni mwetu hawakufika hapo kwa hiyari
yao bali walitengenezwa na binadamu wenzao, ambapo utafiti unaonesha kuwa watu
tunaowaamini na kuwapenda sana ndiyo wenye nafasi kubwa ya kutubandika nembo
mawazo na tabia zao.
Katika hali ya kawaida kila binadamu ana mtazamo wake,
lakini wengi kati yao hawajiamini katika
mienendo yao na
hivyo kuwa tayari kusikiliza na kufuata mitazamo ya wengine bila kulinganisha
na kuhakiki ukweli.
Wengi wetu tulikuwa watu safi kwa sababu tulikuwa na mtazamo wa aina
hiyo.
Lakini kwa mshangao tukajikuta nasi tunaingia taratibu
kwenye tabia za marafiki zetu tukaanza kuiba, kunywa pombe na mambo yafananayo
na hayo.
Tunaweza kujiuliza kwanini tumefikia uamuzi huo? Jibu ni
kwamba tumekubali binadamu wenzetu watupige nembo za uhuni, ujambazi, ukahaba,
ushilikina nk.
Tumekubali kuwaunga mkono wenzetu walioshindwa kujenga ambao
wanatuambia kuwa kwa maisha ya leo ni
vigumu kujenga kwa mshahara mdogo tunaolipwa, na sisi kwa kutokuwa na uwezo wa
kupambanua tunakata tamaa kabisa ya kujiwekea malengo ya kujenga.
Hivi ndivyo binadamu wenzetu wanavyotufanya tuishi kwa
mtazamo na mawazo yao,
tunabadili mitazamo yetu kwa kuiga fikra zao, tunajisikia
vibaya kwa tafsiri zao na wakati mwingine tunaona aibu kwa sababu ya wenzetu
wanavyotusema na kutupachika majina ya hovyo.
Kifupi hivyo ndivyo wanavyotuwekea nembo wenzetu ambao ni marafiki zetu,
ndugu na jamaa zetu tena wakuaminiwa sana.
Uchunguzi unaonesha kwamba asilimia 98 ya binadamu wanaishi
kwa msukumo kutoka kwa watu wengine, lakini jambo baya zaidi ambalo linaweza
kuwa la msingi kufahamu ni kwamba asilimia 89 kati ya hao wanaoathiriwa na
wenzao kwa kupigwa chapa mbaya huku asilimia 11 tu ndiyo ikitajwa kufanikiwa
kwa kufuata mambo mema yafanywayo na wengine. Labda tujiulize kwanini wengi
wetu huathirika kwa sababu ya mitazamo ya wengine na nini cha kufanya? Jibu ni
kwamba tumekuli kuacha kujiamini na kuanza kuishi kwa hofu ya kile
wanachotafsiri wenzetu kuhusu sisi.
Siku zote uwezo ni kitu cha ndani, sasa inakuaje mtu
mwingine atuambie kuwa hatuna uwezo na sisi tumwamini na kunyongea kwa lebo
yake?
Una miaka kumi kazini lakini hata kiwanja huna, hujaanza
kujenga unaogopa ukishindwa watu watakucheka. Unaacha kusoma kwa sababu kuna
mtu/watu wanakuambia hauwezi kufaulu, unakuwa mtumwa wa mapenzi kwa
kumng’ang’ania mpenzi asiyekutaka kwa kuwa unaogopa akikuacha huwezi kumpata
mwingine.
Kamwe usikubali kupigwa lebo na mtu mwingine, simamia imani yako na misimamo yako. Iga mafanikio ya
wengine na si kushindwa kwao kiasi cha kujikuta umekuwa mwizi/jambazi au
changudoa/kahaba sababu ya kumfuata rafiki asiye na dira katika maisha. Hebu
tuache kukubaliana na mitazamo ya wengine kuhusu maisha yetu.
Tuwapuuze wanaotuita majina mabaya, tukatae kufuata mkumbo
na tusikubali kuona aibu kwa mitazamo ya marafiki zetu wa karibu. Maisha ni
sisi tukiweza au tukishindwa wa kuwajibika ni sisi wenyewe.
Kama unataka kufanya kitu
kisicho cha kawaida ni lazima pia ukubali na matatizo yasiyo ya kawaida, na
ufurahie kuyakabili kwani ni shart la maisha.
Pamoja na hayo ili
kuwa salama tunatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa kitu/mtu mwingine yaani
jamii, utamaduni au mazingira yanayotuzunguka.
Kuna mambo lazima yafuatwe, sababu tunaishi na jamii tofauti
ambazo hatufanani nazo vizuri. Ukiacha hilo
utengano wowote unapoteza uhalisia wa jamii nzima.
Mawazo yako ndiyo hukufanya
Uhuzunike.
Lord byron ni mwana falsafa na mshairi mahiri uingereza,
aliwahi kusema kwamba “sanaa kubwa ya maisha ni maono, kuhisi mambo ni madogo
hata katika maumivu”
{The great art of life is sensation, to feel that weexist
even in pain}
Tuchukulie usemi huu kama somo
la kuwafundisha wale wanaolia kwa matatizo mbalimbali maishani. Katika maisha
ya kila siku hayakosekani mambo ya kuumiza.
Kuna kuugua, kufiwa, kukosa chakula, kusalitiwa penzini nk.
Ni mambo ambayo huzaa huzuni na machozi miongoni mwa watu wengi.
Lakini jambo la kujiuliza ni
kwamba tunalia au kuhuzunika kwa sababu matatizo yetu ni makubwa au tumekosa ufahamu
wa maisha.
Hebu tujiulize ni wangapi
tunahuzunikia mishahara midogo tunayolipwa
Kazini kwetu? Je katika huzuni
hizo tushawahi kujiuliza kwamba ni binadamu wangapi hawana kazi? Kama hao wapo sasa ukubwa wa tatizo la kukosa kazi
unaotuliza kila siku uko wapi? Kimsingi uwiano wa shida na uhimili wake unaopatikana
baina ya mtu na mtu haubebi sifa ya
huzuni kuletwa na tatizo kubwa, isipokuwa ni kukosekana kwa sanaa ya kuishi kwa maono na hisia za kupunguza mambo makubwa
kuwa madogo.
Katika hisia mwanadamu hawezi
kuzuia machozi ya furaha au ya huzuni yasitoke.
Ifahamike kwamba kila mwanadamu ana
uwezo wake wa kufanya zaidi ya tatizo analokutana nalo, lakini uwezo huo hauji kama sanaa ya maono na udogoshaji wa matatizo haujapewa
kipaumbele. Kuna watu wanalia kila siku wanahitaji utajiri lakini hawafikii
malengo kwa sababu wanaona umasikini ni jambo kubwa na kuufikia utajiri ni
jambo kubwa pia.
Mtafiti mmoja aitwae William
frey, anasema watu wanalia katika makundi sita tofauti ambayo ni: wenye kujawa
na huzuni zinazosababishwa na matatizo 49% .
Wanaolia kwa furaha ni 21%.
Wanaolia kwa hasira 10%. Wanaolia kwa huruma 7%. Huku wanaolia kwa wasiwasi
ikiwa ni 5%. Wanaolia kwa hofu ni 4%.
Lakini pamoja na kuwepo kwa
makundi hayo sita mwanadamu mwenyewe ana uwezo wa kuyabadili maono yake kwa
kila kundi na kupata matokeo tofauti kabisa, kwani hasira ikipunguzwa kwa kuona
kichocheo kilichojaza hasira hapo kidogo pumzi hushuka na mtu hujiona mwenye
utulivu tofauti na mwanzo.
Vivyo hivyo kwa anayelia kwa
huzuni, huruma, wasiwasi na hofu.
Kwa mantiki ileile hakuna haja ya
kuhuzunika kwa kiwango cha juu wakati kuna kiwango cha chini cha kujiweka huru,
nacho ni cha kutazama mambo makubwa kama
madogo yasiyodumu na kwamba saa, siku, miaka michache ijayo
yatapita. Jiulize hapo ulipo
kinakuliza kitu gani?
Fahamu kwamba hulii au kuhuzunika
kwa sababu matatizo ni makubwa, bali umekosa ufahamu wa maono.
Hebu chukua jukumu la kudharau
shida zako kwa kujilinganisha na wengine ambao bila shaka wanakuzidi. Fanya
hivyo kila unapokabiliwa na tatizo, usilione tatizo ni kubwa kwa takwimu,
lichukulie kuwa ni dogo kisha uanze kulishughulikia utaona linamalizika kwa
ushindi mkubwa.
Kamwe usijaribu kulitatua tatizo
ndani ya maono yanayolikuza kwani hutapata matokeo mazuri. Ukiwa ni umasikini
uone ni mdogo, kufukuzwa kazi, kutokuzaa, kuteswa kwenye mapenzi na matatizo
yote yatakayokukuta katika maisha yako yaone ni madogo kisha tumia nguvu zako
zote kuyakabili hakika utashinda.
Lord byron aliigundua kanuni
aliyoipa jina la Byronic hero, ambayo ilikuwa na misingi ya kuishi kwa maono na
kupunguza ukubwa wa mambo kwa kutumia fikra. Wengi walipata mafanikio makubwa,
kwahiyo jaribu kupunguza matatizo badala ya kuyakuza kwa kuona hayawezekani
kutatuliwa, utaona unashinda matatizo yako kirahisi kabisa.
Kwani binadamu anatakiwa kuamini
kwamba kitu kisichowezekana kama hakikuwa
hivyo basi hakufikiria vya kutosha, kwani unapofikiria vitu kwa vitendo na
kusema haitawezekana, hiyo ni dalili ya kuwezekana kwake lakini na akili yako
inakuwa imefika mwisho wa kufikiri.
Ili kufanya chochote, kuna nguvu
zinazokuunganisha na unachokihitaji.
Ni kutokana na aina ya kufikiri, mazingira na hali ya
kifedha ni kipimo tosha cha kujua ni nini unachowaza, kwani sisi ni matokeo ya
tulichofikiri, na huwa tunaitengeneza dunia kutokana na mawazo yetu.
Hakuna njia nyingine ya kufanyia kazi umakini wetu zaidi ya
hisia za akili ambazo ndio msingi wa kila kitu, ukiufuata msingi huu
utakuwezesha kufanya maajabu katika maisha yako. Kwahiyo jifunze kuongea na
ukimya wako.
SURA YA PILI:
Wewe
ni zaidi ya mwili wako.
Wengi wetu huipa miili yetu nafasi kubwa huku sisi wenyewe
tukifuata nyuma yake.
Tunapoongozwa na miili yetu inamaana kuwa tumetoka kwenye
kufikiri vizuri na kuamia kwenye kufikiri vibaya.
Kwavile miili haina kawaida ya kutafakari wala kukagua hali
halisi, huwa haikubali kurudi nyuma kwenye utashi wala kuzingatia kanuni za
maumbile.
Kama tunajizatiti na kusema
kuwa tunaweza kukaa bila kula wala kunywa chochote kwa siku kadhaa tunaweza.
Tunaweza kwa sababu akili imetutuma kuwa tunaweza.
Tunaweza kufanya yote hayo kutokana na mawazo yetu ya kina.
Dr. Joseph Murphy, katika kitabu chake cha The power of
subconscious mind, anasema: “Unaweza kuyapa maisha yako nguvu zaidi, uwezo
zaidi, afya zaidi furaha na raha zaidi, kwa kujifunza namna ya kuwasiliana na
kutumia nguvu iliyojificha kwenye mawazo yako ya kina” Huu ndiyo ukweli kila
mmoja anaweza kuthibitisha hilo
kwa kufanya.
Lakini kwa upande mwingine inaonesha ni namna gani binadamu
anavyohangaika.
Kuhangaika huku hutufanya tuweze kupambana na wenzetu kusiko
na mwanzo wala mwisho, katika kutafuta kile ambacho tunakiita utajiri, furaha
au amani ya maisha.
Bilashaka tunajifunza kupambana na sio kutafuta njia nzuri
ya maisha, kuishi kwa kujua kanuni ndiyo njia muafaka ya kuwezesha mambo yetu
kwenda kama tunavyotaka.
Kwa maneno mengine tunaweza kusema kama
tunataka kuondoka katika mtego huu na tupate utajiri, afya au furaha ya kweli,
inatubidi tutumie falsafa tofauti.
Katika kufanikisha kile tulichokikusudia, itatubidi tufanye
kwa vitendo yote tutakayoyapata kutokana na falsafa hii mpya. Kama
tunataka kuishi maisha ya utajiri, afya na furaha, inabidi tufuate kanuni
Fulani.
Moja ya kanuni hizo ni kujua kwamba una uwezo usio na
kikomo, na hivi sasa unatumia chini ya asilimia moja ya utajiri wako wa nguvu,
akili na roho.
Badala ya kujisemea moyoni “siwezi” huna budi kujua kwamba
ile nguvu ambayo inauongoza ulimwengu inakuongoza nawe pia.
Amini kwamba nguvu hii hupandisha uwezo wako kutoka asilimia
moja unayoitumia sasa hadi kufikia juu zaidi.
Kanuni nyingine ni kuelewa kwamba ulimwengu huu umeumbwa
kutoka kwenye furaha na siyo kwenye mateso. Ulimwengu asili yake ni furaha ya
ajabu, chochote tukionacho duniani ni furaha ambayo imebadilishwa.
Kama utajifunza kuwaona binadamu, wanyama na vitu vingine
vsivyo na uhai kama furaha kubwa katika umbo
tofauti ni furaha ya ajabu ambayo imebadilishwa tu.
Pia ni muhimu kujua kwamba utajiri mkubwa kuliko wote ni
utajiri wa binadamu, hivyo ni muhimu kujaribu kuuboresha utajiri huo.
Maranyingi tunapozungumzia utajiri wa mali ya nchi, huwa tunazungumzia utajiri wa mali ya asili kama
vile dhahabu, almasi, mafuta na nk. ni muhimu, lakini kiukweli kinachoifanya
nchi iwe tajiri ni utajiri wa watu. Watu wanapokuwa wameelimika ndipo wanapoweza
kuzalisha zaidi.
Mtaji wa masikini ni elimu, huitaji kurithi mapesa mengi ili
uwe tajiri, kwani wapo waliopata pesa huku wakiwa hawana elimu pesa zikapotea
kiajabu tu.
Boresha kwanza ujuzi wako, jichimbue uujue uwezo wako wa
asili, uendeleze uwezo wako na utaweza kufanikisha malengo yako.
Ni jambo la busara kujua kwamba utajiri ni wa kupita tu, jali
kitu ambacho ni cha kudumu. Hakuna ubaya kusumbukia mahitaji yako muhimu ya
kila siku ili uweze kuishi.
Lakini unapaswa kujua kwamba vitu vya duniani si vyako milele
siku moja utatenganishwa na vitu hivyo vya duniani ukiwemo mwili wako.
Wakati unapambana kutafuta mahitaji ya dunia, usisahau
kutafuta utajiri wa kiroho ambao ni wakudumu na hauharibiki wala kupotea.
kumbuka utajiri wa kiroho siyo wa dini, bali kuwakubali
wengine kama walivyo.
Hivi sasa watu wapo kwenye mapambano makali ya kugombea
utajiri wa dunia.
Ukishatambua kwamba dunia ina utajiri wa kumtosha kila
mmoja, fanya jitihada ya kuwapunguzia wengine mizigo yao.
Wasaidie wengine kwa moyo wako wote na isiwe unawasaidia kwa
lengo binafsi la kujinufaisha mwenyewe.
Ukifanya hivyo utaona furaha ya kweli na kwenda hatua moja
mbele kuelekea kwenye dunia ambayo kila mmoja wetu atakuwa tayari kugawana kwa
usawa mali
ya ulimwengu huu. Watu wengi tunapambana kwa sababu hatujui kwamba kwenye
ulimwengu huu kila kitu kipo na hakuna haja ya mtu kupambana ili akipate[Hii
haimaanishi ukae bila shughuli] Ni suala la kujua tu kwamba kuna kanuni Fulani
ambazo mtu akizifuata anaweza kufanikiwa. Kanuni kuu kuliko zote ni ile ya
kufikiri vizuri na kujipenda ili kuwapenda wengine, hapo utabaini njia nyingi
za kumudu kufika utakapo maishani.
Ila ni hadi ujaribu ndipo utakaposhangazwa na matokeo yake, kusoma
tu haitoshi.
Unatakiwa kuamini kwanza kwamba unaweza, kwani uwezo huwa unatoka
nje ya mwili wako.
Nguvu katika Imani
Kwanza kabisa jamii
inapaswa kujua kwamba kuna nguvu nyingi hapa duniani kiasi kwamba hukanganya.
Nguvu hizi zipo chini ya mamlaka ya binadamu kwa sababu nazo zinafuata kanuni
za kimaumbile.
Ni pale tunapozipa nguvu hizi uwezo usio wake ndipo
tunapoingia kwenye kuzifanya zituzidi au kutudhibiti na kututesa.
Moja ya njia za kuziheshimu na kuzijali nguvu hizi ni
kuamini kwamba hazipo kwa ajili ya kuleta uharibifu kwa binadamu. Hata kuibuka
kwa popobawa na vitu vingine vinavyofanana na hilo, havina maana kuwa matukio hayo yanaweza
kutoa uhai wetu.
Bali tunaweza kutoa uhai
wetu kwa kuogopa tu.
Karne hii haipendezi kuendelea kuamini kwamba nguvu yoyote
tusioijua ina maana ya jini au uchawi. Hii ni sababu dunia imeingia mahali
ambapo binadamu amekuwa akigundua haraka uwezo mkubwa alionao.
Sababu binadamu anazungukwa na nguvu nyingi ambazo hazijui
zote, inabidi mtu akiri kwa ufahamu kuwepo kwa nguvu hizi.
Kukiri kwa ufahamu maana yake ni ile hali ya kukubali kuwepo
kwa nguvu za kimawazo bila kuamini kuwa ndani yake kuna nguvu za uchawi, ulozi
au jini vinavyoweza kutengenezwa na jamii Fulani kwa lengo la kumdhuru
aliyekusudiwa.
Cha muhimu hapa ni kujua kuwa kila nguvu iliyomzunguka
binadamu iko chini ya uwezo wa binadamu kama ataamua iwe hivyo, kinachotakiwa
ni kujua tu namna nguvu hizi zinavyofanya kazi na yeye kuishi kwa kufuata
kanuni za kimaumbile ambazo ni pamoja na kuwa na mitazamo na mawazo safi.
Njia rahisi ya kuishi kwa kufuata kanuni za kimaumbile ni
ile ya binadamu kuwa na mawazo na mitazamo minyoofu. Hii ni mitazamo ambayo haimuumizi,
kumvunja nguvu, kumkatisha tamaa au kumtia wasiwasi mhusika na wengine wanaomzunguka.
Hakuna nguvu inayopotea bure, hata nguvu hasi hurudi kinyume
na mtu akadhani amelogwa sababu maelezo ya kuhalalisha kupatwa kwake na nguvu
hizo hasi yanaweza kukosekana. Nguvu hizi hasi zinaweza kutengeneza matukio na
kubuni madude yenye maumbo wa majini na popobawa.
Kila mmoja wetu ana nguvu ndani yake ambazo ni kubwa sana.
Nguvu hizi kwa sehemu kubwa ziko kwenye mawazo yetu.
Namna tunavyojitazama, kujiamini kutafsiri matukio,
kuwatazama wengine na mazingira, hufanya tofauti kubwa kati yetu.
Itakuwa ni kama ndoto kwetu kukumbana na jini, uchawi na
vitu vinavyofanana na hivyo kama tutatumia nguvu
hizi tulizonazo vizuri.
Tukijua kwamba tuna nguvu hizi ambazo hupaliliwa na kukuzwa
na namna tunavyoweza kuishi kwa kufuata kanuni za kimaumbile, hatuwezi
kudhuliwa wala kuogopeshwa na matukio yanayohusisha uchawi. Jamii inaweza
kuishi bila kutengeneza dhana ya vitu vya ajabu ambavyo kwa akili ya kawaida tu
haviwezi kuleta hofu.
Uchawi ni istilahi tu, haina maana yoyote yenye kushikika.
Hii inamaana kwamba uchawi siyo kitu Fulani maalum, bali ni dhana pana lakini
yenye kulenga uharibifu.
0 comments:
Post a Comment