Friday, February 26, 2016

Sababu ya kukoroma na jinsi ya kuzuia hali hiyo.

Sababu ya kukoroma na jinsi ya kuzuia hali hiyo
Kukoroma ni tatizo linalowapata watu wengi wakati wanapolala ambalo linaweza kuwatokea watu wa kila umri ingawa hutokea mara nyingi kwa wanaume au watu wanene. Kukoroma huzidi kwa kadri umri unavyoongezeka na asilimia 54 ya watu wazima hukoroma baadhi ya wakati huku asilimia 25 ya wengine wakiwa na tabia ya kukoroma kila wakati. Kukoroma baadhi ya wakati kwa kawaida sio tatizo kubwa na mara nyingi huleta tu karaha kwa mtu anayelala karibu na mkoromaji. Hata hivyo kukoroma huko sio tu kwamba huharibu usingizi wa anayekoroma bali pia huwasumbua na kuwakeresha wanaolala karibu na mkoromaji. Wale wenye tabia ya kukoroma, hukoroma kila wanapolala na mara nyingi huchoka wanapoamka, na watu wa aina hii hushauriwa kumuona daktari na kushauriwa kuhusiana na tatizo hilo. Lakini kabla hatujaendela mbele ni bora tujue kukoroma hasa ni nini au hutokea vipi?
Mtu huwa anakoroma pale kunapokuwa na kitu au sababu yoyote itakayoziba kuingia au kutoka kwa hewa mdomoni na katika pua. Kuta za koo hutikisika wakati wa kupumua na matokeo yake ni sauti inayosikika ya kukoroma. Kuingia au kutoka kwa hewa huweza kuzuiwa na sababu mbalimbali kama vile:
• Kuziba tundu za pua kusiko kamili ambako husababisha nguvu zaidi zitumike katika kupitisha hewa kwenye pua wakati mtu akiwa amelala. Kitendo hicho hupelekea nyama laini za pua na koo zijikusanye na kusababisha mkoromo. Kuna baadhi ya watu wanakoroma tu kipindi cha allergy (allergy season) au wanapatwa na matatizo ya sinus. Baadhi ya matatizo kama vile kupinda pua (deviated septum) au ukuta unaotenganisha tundu za pua na polyps za pua pia huweza kufanya pua zizibe na kusababisha kukoroma. Watu wengi wanaofanya operesheni za pua pia hupatwa na tatizo la kukoroma.
• Kuwa na misuli dhaifu katika koo na ulimi. Misuli au nyama za koo na ulimi zinapokuwa dhaifu sana hulegea na kuanguka upande wa nyuma wa sehemu inayopita hewa. Suala hilo hutokea pale mtu anapolala fofofo au kuwa na usingizi mzito na kusababisha kukoroma.
• Kuwa na misuli minene ya koo. Hii ni kwa wale watu wanene ambao hata nyama zao za koo pia hunenepa na kupanuka na suala hilo husababisha kukoroma, Pia watoto wenye tonsesi kubwa na adenoids baadhi ya wakati hukoroma.
• Kuwa na kilimi kikubwa ni mojawapo ya sababu zinazosababisha kukoroma. Kilimi kirefu kinaweza kuzuia koo na pale kinapotikisika wakati hewa inapita kwa msukumo husababisha kukoroma.
• Sababu nyinginezo zinazoweza kumsababishia mtu akorome anapolala ni kuwa na umri mkubwa au uzee, imeshuhudiwa kuwa watu wa makamo na wazee hukoroma, kwani misuli na nyama za koo huanza kuzeeka na kulegea kadri umri unayoongezeka. Vilevile wanaume wanakoroma zaidi kuliko wanawake hii ni kutokana na wanaume kuwa na njia nyembamba zaidi ya hewa kuliko wanawake. Kukoroma pia kunaweza kuwa ni tatizo la kurithi. Pombe, kuvuta sigara na matumizi ya baadhi ya dawa pia husababisha misuli ya koo ilegee na hivyo hupelekea mtu akorome. Kulala vibaya pia husababisha kukoroka kama vile kulala kichalichali, kwani hufanya nyama za koo zilegee na kuziba hewa.
Je, Dawa ya kukoroma ni nini?
Swali hilo limeuliwa sana na mimi katika kulijibu ningependa kusema kuwa, kujua sababu inayosababisha mtu akorome na kuitatua au kuiondoa sababu hiyo ndiko kunakotibu kukoroma. Sote tunajua adha inayotokana na kukoroma, na sauti hiyo inavyosumbua hasa iwapo anayekoroma ni mtu wako wa karibu kama vile mumeo, mwenzi wako au yoyote yule inayekubidi ulale naye karibu au katika kitanda kimojana hata chumba kimoja. Kukoroma pia huathiri usingizi wa mkoromaji kwani anayekoroka humbidi aamke mara kadhaa usingizini akijua au bila kujua kutokana njia zake za hewa kufunga kwa sekunde kadhaa ambapo usingizi pia hukatika. Wanaokoroma pia hushindwa kulala vizuri suala linalopelekea asubuhi wawe wamechoka na kutofanya majukumu yao vyema, na pia wale wanaolala nao karibu hupatwa na matatizo kama hayo. Vilevile tunapaswa kujua kuwa kukoroma kuna athari za kiafya za muda mrefu kwa mtu anayekoroma hivyo si jambo la kufanyia mzaha na ni tatizo ambalo linapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa.
Wataalamu wanatuambia kuwa ili kujua kukoroma kwako kunasababishwa na nini ni bora ushirikiane na mwenzi wako au yoyote unayelala naye ili akuchunguze pale unapolala na kujua jinsi mwili wako unavyokuwa pale unapokoroma. Ni bora aandae orodha na kuchunguza yafuatayo:
1. Kufunga mdomo na kukoroma kunaonyesha kuwa kuna matatizo ya ulimi.
2. Kufungua mdomo na kukoroma kunaonyesha unaweza kuwa na tatizo katika misuli au nyama za koo.
3. Kukoroma unapolala kichalichali kunaonyesha kuwa pengine kwa kubadilisha namna unavyolala kukoroma nako kunaweza kwisha.
4. Kukoroma wakati unapolala kwa kila mlalo kunaonyesha kwamba tatizo lako ni kubwa na pengine kunahitajia tiba kubwa zaidi.
Iwapo umebadilisha namna unavyolala na haikusaidia, unashauriwa ujaribu yafuatayo:
 Punguza uzito
 Safisha njia yako ya hewa. Kuwa na pua iliyoziba hufanya kupumua kuwe kugumu na kusababisha kukoroma. Unaweza kufanya hivyo kwa kutumia dawa za kusaidia kupumua kwa urahisi (nasal decongestants) zinazopatikana kwa urahisi katika maduka ya dawa.
 Wacha kuvuta sigara.
 Lala mapema na pata usingizi wa kutosha kila mara huku ukijiepusha na kuchoka sana. Kunyanyua kichwa kwa nchi 4 huweza kupunguza kasi ya kupumua na kusaidia ulimi na taya kwenda mbele hali ambayo hupunguza kukoroma. Fanya hilo kwa tumia mito maalum ya kupunguza kukoroma au lala bila mto.
Wataalamu pia wanasema kwamba unaweza kupunguza kukoroma kwa kutokula baadhi ya vyakula au dawa kabla ya kulala ambavyo huongeza kukoroma. Vitu hivyo ni kama vile
o Kutokula mlo mkubwa kabla ya kulala.
o Kutokula vyakula vinavyotokana na maziwa au maziwa ya soya.
o Kutokunywa pombe kabla ya kulala.
o Kutotumia dawa aina ya antihistamines.
o Kutotumia vyakula au vinjwaji venye kafeini.
Vilevile wanaokoroma wanashauriwa kufanya mazoezi ya koo ambayo ni pamoja na kuimba, kusoma kwa kurudia rudia voweli (a,e,i,o,u) kwa nguvu kwa dakika tatu mara kadhaa kwa siku, kuweka ncha ya ulimi chini ya meno ya mbele na kurudisha ulimi nyuma kwa dakika 3 kila siku au huku mdomo ukiwa wazi pelekea taya yako upande wa kulia na wacha ibakie katika hali hiyo kwa sekunde 30. Huku mdomo ukiwa wazi, kaza misuli ya nyuma ya koo na rudia kitendo hicho kwa sekunde thelathini. Unaweza kutizama kwenye kioo na kuona jinsi kilimi kinavyokwenda juu na chini.
Iwapo kukoroma hakutoisha kwa kutumia njia hizo tofauti zilizoelezwa, usife moyo jaribu kumuona daktari na akupe ushauri wa kitiba kuhusiana na tatizo hilo. Madakatari wataalamu wa magonjwa ya pua, masikio na koo au ENT wanaweza kukusaidia zaidi kutatua tatizo hilo. Siku hizi kuna vifaa mbalimbali vinavyotumiwa mahospitalini ili kuondoa kukoroma kama vile kifaa kinachowekwa kwenye meno, CPAP, kidude kinachowekwa mdomoni au hata kufanyiwa operesheni ili kuondoa tatizo hilo.

KUOTA UPALA/UWALAZA- FAHAMU CHANZO NA TIBA YAKE


Siku hizi ni jambo la kawaida sana kuona vijana wa umri wa miaka 20 hadi 35 wakiota Upara. Fanya uchunguzi mdogo tu huko mitaani utagundua vijana wadogo haswa wa kiume wanaota vipara mapema sana kuliko kawaida. Na wengi tunaamini kuwa Upara ni ishara ya busara ama kufanikiwa kimaisha. Leo katika makala hii utaweza kufahamu nini chanzo cha upara katika umri mdogo na ni nini tiba yake. ningependa kukuhakikishia mapema kuwa tiba ipo na haina gharama yoyote.
kikawaida kwa binadamu yeyote iwe mwanamke ama mwanaume huanza kupoteza nywele kichwani kwa kasi kuanzia miaka ya 50 na kuendelea kutoka na kuchoka kwa mwili. Ni swala linalokasirisha sana kwa kijana mdogo kuota upara angali bado unazihitaji nywele.
Haikubaliki
Upara ukuingiapo huanza taratibu taratibu, mwanzoni huwezi kugundua kuwa ni upara unaokunyemelea, utahisi ni matatizo madogo madogo tu ya nywele. kwa mtu ambaye hana kawaida ya kuchunguza nywele zake kwa ukaribu itaweza kuchukua miaka 2 au zaidi kugundua tatizo.
Inafka wakati nywele zinakuwa zimepukutika kwa kiasi kikubwa sana ndipo untambua kwamba hiki ni kipara. inakela sana na usiombe uwe na kichwa chenye umbo baya, uzuri wa sura wote hutoweka na utatamani hata uvae vigi ama ushonee wiving. Ukifikia pointi hii ndipo utapogundua kuwa nywele ni muhimu sana na ni urembo tosha wa binadamu.
Kwa mtu ambaye hajapatwa na hili tatizo hawezi kuona uzito wa hili swala, nina imani vipara vinawakela wengi sana. Na ni vijana wachache sana walio huru na vipara vyao, nao ni wale tu wenye vichwa vyenye umbo zuri ama ni wale wasiojari muonekano wao. Kundi lililobaki wote wanatamani miujiza itendeke vichwa vyao viweze kuotesha nywele tena..
Nadhani leo ni nafasi nzuri kwako kufahamu ni nini chanzo cha vipara kwa vijana wenye umli mdogo na namna ya kutibu. zipo sababu nyingi sana. na kwa kijana yeyote iliye na upara atakuwa amekumbwa na sababu moja wapo ama mbili kati ya hizi nitakazo kueleza
CHANZO/SABABU ZA KUOTA UPALA KATIKA UMRI MDOGO
Lishe duni,
Nafasi kubwa ya nywele imajengwa kwa protini, pia kuna virutubisho vingine vingi vinavyosaidia uzalishaji wa nywele, kama madini ya zinki, chuma, potasiamu, vitamin E, B, C na hewa ya oksigeni. virutubisho hivi tunavipata kutokana na vyakula tunavyokula kila siku. baada ya kuliwa, virutubisho hivi husambazwa kwenye ngozi ya fuvu la kichwa (Scarp) kwa njia ya damu. Mtu yeyote akikosa virutubisho hivi kwa kiwango kinachotakiwa lazima atapatwa tatizo la kupukutika kwa nywele.
Tambua kuwa madawa na mafuta mengi ya nywele tunayoyatumia hutengenezwa kwa tutumia vyakula vyenye virutubisho hivi, hakuna uchawi mwingine. Katika Makala ijayo nitakueleza kwa undani zaidi ni vyakula gani unavyopaswa kula ili uweze kuwa na nywele nzuri, wala hakuna haja ya kuhangaika na madawa.

Msongo wa Mawazo. (Stress),

Msongo wa mawazo ni chanzo king I one kikubwa sana cha tatizo la nywele na ndicho haswa kinachowakumba vijana wengi wa sasa na kuwasababishia vipara katika umri mdogo. Kitaaramu imegundulika kuwa msongo wa mawazo unaathiri mzunguko wa damu kwenye ngozi ya vuvu la kichwa hivo damu hushidwa kufikisha virutubisho na hewa ya kutosha kwa ajiri ya uzalishaji wa nywele.
Kikawaida binadamu anapokuwa anawaza sana misuli iliyozunguka fuvu la kichwa kusinyaa na kukunjamana kitu ambacho husababisha ngozi na mishipa midogo midoho ya damu kusinyaa na kukunjamana pia hivyo damu inashidwa kupenya na kusambaa kwa urahisi katika maeneo yote ya ngozi ya kichwa kitu kinachopelekea upungufu wa virutubisho na hewa kwa ajili ya ukuaji wa nywele na hatimaye nywele huanza kudhoofika. baadhi ya wasomi na watu wanaopigana sana na ugumu wa maisha hupata vipara kwa njia hii.
Matatizo katika mfumo wa homoni,

Homoni zinahusika sana na kukuaji wa nywele. Upugnufu ama madiliko katika homoni husababisha kudhoofu kwa nywele, kuna sababu nyingi zinazoathiri mfumo wa homoni, mfano Magonjwa, Ujauzito, mwili kukosa hewa ya oksigeni yakutosha pamoja na uvutaji wa sigara.
Kurithi toka kwa wazazi,
Pia inaaminika bainadamu anaweza kurithi tatizo la upara kutoka kwa kizazi chake kilichotangulia. Lakini hapa huwa najiuliza sana sabubu kuna baadhi ya watu wamepata vipara wakati kwenye ukoo wao hakujatokea mtu mwenye upara.
Baada ya kufahamu chanzo cha upara, Sasa unahitaji kufahamu namna ya kutibu tatizo.
Najua niechukua muda wako mwingi sana kuipitia makala hii lakini naamini umejifunza kitu. Katika makala nitakayokuandalia kesho ilazungumzia kiundani namna ya kutatua tatizo la upara.kwa leo inatosha najua utachoka kusoma. Nakuhakikishia kuwa kutibu upara inawezekana tena kwa kutumia vyakula na dawa zetu za asili ambazo naamini zinapatikana katika kila nyumba hapa kwetu Tanzania. Nitakueleza namna ya kutengeneza dawa hizi. Zimewasaidia wengi ingawa bado hazijafahamika sana.

Saturday, February 20, 2016

MARUFUKU MISHIKAKI KATIKA BODABODA

By Frank Geofrey, Jeshi la Polisi

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi litaanza kuwachukulia hatua waendesha pikipiki wanaobeba zaidi ya mtu mmoja, kupita wakati wa taa nyekundu na wasiovaa kofia ngumu.
Ubebaji wa abiri zaidi ya mmoja, maarufu kwa jina la mishikaki, umeenea karibu mikoa yote kutokana na wananchi wengi kuona unawapunguzia gharama.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu ametoa maagizo hayo kwa makamanda wote nchini wakati akizungumza na maofisa wakuu wa polisi, wakiwamo wa mikoa, vikosi na makao makuu katika kikao kazi kilichomalizika Dar es Salaamjana.
IGP Mangu alisema kwa muda mrefu, waendesha bodaboda wamekuwa wakivunja sheria za usalama barabarani, lakini sasa mwisho wao umefika na kuwataka makamanda wa mikoa yote nchini kutekeleza maelekezo hayo ili kujenga nidhamu kwa bodaboda.
Mkuu huyo alisema suala la kufuata sheria za usalama barabarani kwa bodaboda halina mjadala na kila kamanda ahakikishe kuwa wale wote wasiofuata sheria na kukaidi, wanakamatwa kwa kuwa wamekuwa wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.
“Pamoja na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo kwa kila mkoa kuhakikisha unaendesha oparesheni kali dhidi ya bodaboda ili kupunguza ajali zinazosababishwa na wale ambao wengi wao hawataki kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani,” taarifa ya Jeshi la Polisi inamkariri IGP Mangu.
“Tusiwaonee muhali maana maisha ya watu ni muhimu sana na jambo la msingi ni kusimamia sheria tu.”
Awali, akifungua kikao kazi hicho, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea na mapambano yake dhidi ya uhalifu na wahalifu ili usalama wa raia na mali zao uendelee kuimarika na wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo bila hofu ya uhalifu.

Friday, February 19, 2016

Anasa za kidunia

Kijana wa kiume alimwambia baba yake "nimemuona msichana mzuri sana na ninataka nimuoe hivi karibuni. Ni mzuri sana na ana macho mazuri mno" baba akamwambia sawa mwanangu mlete nyumbani umtambulishe.
Kijana alimleta yule msichana nyumbani, baba alikubali uzuri wa yule binti na kumwambia mwanae "mwanangu hustahili kuwa na msichana huyu. Binti kama huyu anastahili kuwa na mtu mwenye uzoefu wa maisha na anayeweza kumtegemea. Mtu kama mimi"
Kijana alishangaa msimamo wa baba yake na akamwambia "nitamuoa mimi na sio wewe baba" na ghafla wakaanza kugombana, na baadae wakaamua kwenda police kusuruhisha.
Walipomuelezea afisa wa polisi tatizo lao, yule afisa akawaambia wamlete huyo msichana kwake wamuulize yeye anamhitaji nani. Afisa alipomuona yule msichana akawageukia baba na mtoto na kuwaambia "wote ninyi hamfai kuwa na msichana huyu, anahitaji mtu aliye juu kama mimi, mtu ambaye ana nguvu za kuweza kumlinda."
Wote watatu wakaanza kuzichapa, na baadae mkuu wa kituo akatokea. Mkuu wa kituo akawauliza wanagombania nini na wote kwa pamoja wakamuonesha mkuu wa kituo yule binti. Mkuu alipomuona binti akawaambie "nyie wote ni wapumbavu, msichana mzuri kama huyu afaa kuwa mke wa mkuu wa kituo! Ondokeni hapa na mniachie huyu binti niongee nae"
Wote wanne wakaanza kugombana tena, mwishoni yule binti akawatuliza na kuwaambia "me nina ufumbuzi wa huu mgogoro wenu nitaanza kukimbia, yeyote atakayefanikiwa kunikamata atakuwa mme wangu" alipoaanza kukimbia wote wanne wakaanza kumfukuzia ili kumkamata ma ghafla wote wanne wakatumbukia katika shimo kubwa.
Binti akawatazama tokea juu ya lile shimo na kuwaambia "mnajua mimi ni nani? Mimi ni ulimwengu huu. Watu wanakimbia kweli kunikamata au kwenda sambamba na mimi, kwa kufanya hivyo wamemsahau hata Mungu mpaka pale wanapoingia kaburini wamekufa bila ya kuweka uhusiano mzuri na Mungu! Yote ni kwa ajili ya uzuri tu wa mimi! Nawaambieni tu Mungu yupo! Msitazame uzuri wa ulimwengu huu mkamsahau Mungu.
Muhimu.
Usimsahau mwenyezi Mungu, anakupigania unapumua mpaka leo hii, usizubaishwe na anasa za ulimwengu huu! Mfalme Sulemani alisema vyote ni ubatili mtupu.
Kwanini usiseme AMEN!??