Saturday, February 20, 2016

MARUFUKU MISHIKAKI KATIKA BODABODA

By Frank Geofrey, Jeshi la Polisi

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi litaanza kuwachukulia hatua waendesha pikipiki wanaobeba zaidi ya mtu mmoja, kupita wakati wa taa nyekundu na wasiovaa kofia ngumu.
Ubebaji wa abiri zaidi ya mmoja, maarufu kwa jina la mishikaki, umeenea karibu mikoa yote kutokana na wananchi wengi kuona unawapunguzia gharama.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu ametoa maagizo hayo kwa makamanda wote nchini wakati akizungumza na maofisa wakuu wa polisi, wakiwamo wa mikoa, vikosi na makao makuu katika kikao kazi kilichomalizika Dar es Salaamjana.
IGP Mangu alisema kwa muda mrefu, waendesha bodaboda wamekuwa wakivunja sheria za usalama barabarani, lakini sasa mwisho wao umefika na kuwataka makamanda wa mikoa yote nchini kutekeleza maelekezo hayo ili kujenga nidhamu kwa bodaboda.
Mkuu huyo alisema suala la kufuata sheria za usalama barabarani kwa bodaboda halina mjadala na kila kamanda ahakikishe kuwa wale wote wasiofuata sheria na kukaidi, wanakamatwa kwa kuwa wamekuwa wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.
“Pamoja na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo kwa kila mkoa kuhakikisha unaendesha oparesheni kali dhidi ya bodaboda ili kupunguza ajali zinazosababishwa na wale ambao wengi wao hawataki kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani,” taarifa ya Jeshi la Polisi inamkariri IGP Mangu.
“Tusiwaonee muhali maana maisha ya watu ni muhimu sana na jambo la msingi ni kusimamia sheria tu.”
Awali, akifungua kikao kazi hicho, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea na mapambano yake dhidi ya uhalifu na wahalifu ili usalama wa raia na mali zao uendelee kuimarika na wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo bila hofu ya uhalifu.

0 comments:

Post a Comment